Abstract:
Kiswahili ni lugha pekee ya Kiafrika ambayo imejinyakulia nafasi ya juu
miongoni mwa lugha za kimataifa. Imefikia umataifa huu kutokana na kuenea
kwake kijiografia na kimatumizi ndani na nje ya Afrika Mashariki, eneo
ambalo ni kitovu chake cha pili hasa cha Kiswahili Sanifu ambayo ni lahaja
inayokuzwa kimataifa. Kitovu chake cha kwanza hasa kwa lahaja zake asilia
kikiwa mwambao mwa Afrika. Uenezi huu umekuwa wa kasi baada ya nchi
za Afrika Mashariki - Tanzania, Uganda na Kenya - kupata uhuru mwanzoni
mwa miaka ya 1960. Uhuru huu ulifanya Kiswahili kuenea katika eneo hili
hadi kujitwalia hadhi ya kuwa lingua franka. Nchi hizi huru ziliinua hadhi ya
Kiswahili kwa njia tofauti; Tanzania iliifanya lugha rasmi, Kenya lugha ya
taifa, na Uganda lugha rasmi kwa amri ya Rais mnamo mwaka 1973
(Pawlikova-Vilhanova, 1996). Japo amri hii ya Rais haijatekekezwa hadi sasa,
Kiswahili bado kinatumika nchini Uganda kama lugha ya jeshi na polisi na
kama lingua franka katika mitagusano ya kibiashara na kijamii. Hadhi hii
imesaidia kuenezea Kiswahili ndani na nje ya Afrika. Japo uenezi huu una
motisha, haibainiki wazi jinsi shughuli za ujenzi wa mataifa haya zilivyokuza
uenezi wake hadi kuufikisha kiwango cha kimataifa katika miongo mitano
pekee ikizingatiwa kuwa, si nchi zote zilizoweka mikakati ya kuikuza. Kwa
kuwa uenezi wake umefungamana na shughuli za kimaendeleo katika mataifa
haya, makala hii imechunguza uenezi wake kwa mtazamo wa Nadharia ya
Mifumo Changamano.